HABARI

LUIS MIQUISSONE AINGA ANGA ZA WAARABU WA MISRI, SIMBA YAFUNGUKA

 


 LUIS Miquissone nyota wa kikosi cha Simba huenda msimu ujao asiwepo kwenye kikosi hicho kinachoshiriki Ligi ya Mabingwa Afrika kikiwa hatua ya makundi baada ya mabosi wa Al Ahly Waarabu wa Misri kutajwa kuhitaji saini yake pamoja na Klabu ya TP Mazembe ya Congo.

Al Ahly walitambua balaa lake kupitia mchezo wao wa hatua ya makundi uliochezwa Uwanja wa Mkapa, Februari 23 na kupokea kichapo cha bao 1-0 Uwanja wa Mkapa.

Bao pekee la ushindi kwa Simba lilifungwa na kiungo huyo akiwa nje ya 18 kwa guu lake la kulia akitumia pasi ya Clatous Chama.

TP Mazembe ya Congo wao walimuona kwenye mashindano ya Simba Super Cup, ambayo ilifanyika Uwanja wa Mkapa na nyota huyo kuonyesha uwezo wake.

Pia mashabiki wa timu hiyo ambayo anacheza pia Mtanzania Thomas Ulimwengu walionekana kuukubali uwezo wa nyota huyo na kuwaomba viongozi wao wafanye mchakato kupata saini yake.

Mbali na Al Ahly kumuona kwenye mchezo huo wa Ligi ya Mabingwa Afrika pia Kocha Mkuu wa Al Ahly, Pitso Mosimane ameweka wazi kwamba anamtambua vema Luis na alimfuatilia kwenye mchezo dhidi ya AS Vita nchini Congo wakati Simba ikishinda bao 1-0.

Mosimane amesema:”Ninamtambua Luis ni moja kati ya wachezaji wazuri, hata kabla ya mchezo wetu niliwaambia wachezaji wangu kwamba wanakutana na wachezaji wenye uwezo mkubwa ndani ya uwanja ikiwa ni pamoja na Luis.

“Hivyo ninapenda kuona kazi yake ndani ya uwanja na ni moja kati ya wachezaji ambao walitupa changamoto kubwa katika mchezo wetu,”.

Kuhusu suala hilo la kuhitaji saini yake, Ofisa Habari wa Simba, Haji Manara amesema kuwa anatambua kuwa kwa sasa kuna timu nyingi duniani ambazo zinahitaji saini ya nyota huyo.

“Unajua kwa sasa ipo wazi duniani kote kuna mawakala ambao walikuwepo Uwanja wa Mkapa na wale ambao wanafuatilia mpira, Luis kwa sasa yupo sokoni na anahitajika achana na Afrika na nje ya Afrika pia.

“Hivyo kwa kuwa yeye ni mchezaji ikitokea timu ikahitaji saini yake ni lazima ijipange kumpata kwa kuwa ni moja kati ya wachezaji ghali na ni mzuri hivyo mazungumzo yatafanyika na kila kitu kitakuwa sawa,” .

About the author

kidevu

Leave a Comment