HABARI

SIMBA YALIVALIA NJUNGA SUALA LA SENZO NA AL AHLY

 

 UONGOZI wa Simba umesema kuwa jambo ambalo amefanya Senzo Mbatha la kukutana na Kocha Mkuu wa Al Ahly, Pitso Mosimane sio la kiungwana na hakupaswa kufanya hivyo.

Usiku wa Februari 22, picha za Mbatha ambaye alikuwa Mtendaji Mkuu ndani ya Simba,(CEO) kabla ya kubwaga manyanga na sasa yupo ndani ya Yanga akiwa ni Mshauri Mkuu wa Masuala ya Mabadiliko  zilisambaa akiwa na Mosimane siku moja kabla ya kuvaana na Simba kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa hatua ya Makundi.

Mchezo huo ambao ulichezwa jana, Februari 23, Simba ilishinda bao 1-0 kupitia kwa Luis Miquissone ambaye aliitendea haki pasi ya Clatous Chama.

Ofisa Habari wa Simba, Haji Manara akizungumza na +255Global Radio amesema kuwa kwa mtu muungwana hakupaswa kufanya hivyo kwa kuwa Simba inapambana kwa ajili ya taifa la Tanzania.

“Naskia watu wanasema kwamba alikuwa amekwenda kukutana na Msauzi mwenzake (kwa kuwa Senzo na Misomane ni raia wa Afrika Kusini), ila ninaamini kwamba sio sawa.

“Inaelezwa alianza kusema kwamba alitaka kuonana naye siku ya Ijumaa ila akakwama na kuamua kuchagua Jumatatu, hapana kwa nini iwe siku moja kabla ya mechi?

“Ingekuwa yupo ndani ya Simba angeweza kufanya hivyo? Sisi huwa tunaonana nao kwa mujibu wa taratibu kwa kuwa kuna muda wa kufanya vikao vile kabla ya mechi hapo tunaongea na kubadilishana mawazo kwa kuwa mpira sio vita.

“Kikubwa ninawaambia mashabiki wawe na subira unapozungumza kuhusu Simba unazungumzia taasisi kubwa yeye watu wengi, sasa tunafanya vitu vyetu kwa umakini mkubwa,” amesema.


About the author

kidevu

Leave a Comment